Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa Mradi wa Kujenga na Kuimarisha Ushirikiano wa Kikanda wa Afrika Mashariki (EASTRIP) ni muhimu kwa kuwa una kwenda kusaidia katika utekelezaji wa mabadiliko ya kielimu ambayo yameaanza kutekelezwa kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014, Toleo la 2023 pamoja na Mitaala mipya katika ngazi mbalimbali.



Prof. Nombo ameyasema hayo Julai 30, 2024 Mkoani Kilimanjaro wakati wa Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Chuo cha Ufundi Arusha Kampasi ya Kikuletwa Wilayani Hai ambapo amesema kuwa 'Mradi huo umeshirikisha nchi tatu za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Kenya na Shirikisho la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ethiopia ambazo kwa ujumla zinatekeleza mradi kwa kuanzisha vituo vya umahiri kumi na sita (16).



Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa Mradi wa EASTRIP unatekelezwa kuendana na miradi ya kimkakati ya Kitaifa na umetengewa jumla ya Dola za Kimarekani milioni 75 sawa na shilingi Bilioni 187.5 kwa ajili ya kuanzisha Vituo vinne vya umahiri nchini katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na Chu cha Teknolojia Dar es Salaam ambacho kina Vituo viwili vya Umahiri.