
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu.

Akizungumza katika hafla ya utoaji tuzo iliyofanyika jijini Dar es Salaam , Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetenga jumla ya shilingi bilioni 4.2 kwa kipindi cha miaka minne tangu kuanzishwa kwa tuzo hiyo ambazo zimetumika kugharamia uendeshaji wa tuzo, kuchapisha vitabu vilivyoshinda na kutoa zawadi kwa washindi katika nyanja mbalimbali.

“Hakika tunamshukuru sana Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipatia Wizara fedha kwa ajili ya uendeshaji wa Tuzo hii,” amesema Prof. Nombo.
Aidha, ameongeza kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imepanga kushirikiana na vyuo vikuu na idara za fasihi kuendesha warsha kwa waandishi chipukizi na kongamano la kitaifa la uandishi bunifu Ili kuongeza hamasa ya uandishi na kukuza sekta ya uchapishaji nchini.

Prof. Nombo amesisitiza kuwa uwekezaji huu umechangia si tu kuongeza ari ya waandishi, bali pia umeimarisha sekta ya uandishi na uchapishaji ambayo ni moja ya malengo makuu ya tuzo hiyo.
Katibu Mkuu huyo ametoa wito kwa Watanzania kuendeleza utamaduni wa kusoma na kuandika vitabu ili kuunga mkono juhudi za Serikali.

