Wananchi wa Kata ya Msingisi wilayani Gairo Mkoani Morogoro wameishukuru Serikali kwa kuwajengea VETA Gairo na kuiomba kuikamilisha ili vijana wa eneo hilo waweze kukitumia Chuo hicho kupata ujuzi.



Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya elimu, utamaduni na michezo Machi 18, 2026 katika VETA hiyo wamesema wana shauku kubwa kuona VETA hiyo inakamilika na kuanza kutoa mafunzo.



Diwani wa Kata ya Msingisi Mhe. Daudi Mwegalawa amemshukuru Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwapatia VETA katika wilaya hiyo akisema itakuwa mkombozi kwa wakazi wa eneo hilo katika kupata ujuzi na ajira.



Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya elimu, utamaduni na michezo amewataka wanachi wa eneo hilo kuwa na amani na kwamba Kamati yake itafuatilia kuhakikisha fedha zinapatikana ili VETA hiyo na zote zinazojengwa zinakamilika kwa wakati ili wanachi wafaidike nazo.



"Tunataka VETA zote zinazojengwa zikamilike kwa wakati, Rais alishatoa idhini ya fedha na sisi tulipitisha Bajeti kwa nini fedha hizo haziji, tunaomba Wizara leteni taarifa ya mtiririko fedha na hatua za utekelezaji wa miradi hii 65 ili tufuatilie ikamilike," amesema Mhe. Sekiboko.



Ujenzi wa VETA hizo 65 awamu ya kwanza unahusisha majengo ya Utawala, karakana, Nyumba za walimu, madarasa, Maliwato, ofisi ya mlinzi na Nyumba ya umeme