Serikali inaendelea na maandalizi ya kupokea idadi kubwa ya wanafunzi kidato cha kwanza mwaka 2028 kutokana na makundi rika mawili (double cohort)


Moja ya mkakati ni ushirikiano na sekta Binafsi na Ili kufanikisha hilo Serikali itaendelea kujadili kwa karibu na wamiliki wa shule binafsi ili kwa pamoja kupanga mipango ya utekelezaji.



Akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo visivyo vya Serikali Tanzania (TAMONGSCO) jijini Dodoma Aprili 15, 2026 Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Wanu Hafidh Ameir amesema tayari tathmini imeonesha uhitaji wa miundombinu ni takribani madarasa mapya laki tano ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi hao na kwamba katika kufanikisha hilo Serikali imeandaa mkakati wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP).



“Sekta binafsi imeendelea kuwa mhimili muhimu katika kuboresha elimu kwa kuongeza fursa na ubora, tutaendelea kuimarisha ushirikiano huo zaidi ili kukuza sekta kwa tija na ufanisi. Nitoe rai kwenu tuendelee kushirikiana ili maandalizi ya Double Cohort mwaka 2028 yafanikiwe,” amesisitiza Mhe. Wanu.



Naibu Waziri Wanu ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maelekezo yake kwa Wizara yanayochochea mageuzi katika sekta ya elimu, hasa katika kuimarisha masomo ya sayansi na stadi za kazi ili ziendane na soko la ajira.