
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezindua na kukabidhi vifaa vya kisasa vya TEHAMA kwa shule za Amali 19 nchini, ikiwa ni hatua ya kuimarisha elimu ya vitendo ili kuwajengea wanafunzi umahiri kwa njia kidigitali.

Akizungumza katika uzinduzi huo jijini Dodoma Mratibu wa Mafunzo ya Kidigitali Wizara ya Elimu Dkt. Alcardo Alex amesema baadhi ya vifaa hivyo ni mashine za uhalisia pepe (Virtual Reality – VR) ambazo zitasaidia wanafunzi kufanya mafunzo kwa vitendo bila kutumia vifaa halisi, na hivyo kuongeza uwezo wao wa kujifunza mara kwa mara bila hofu ya madhara.

Dkt. Alcardo amesisitiza kuwa teknolojia ya uhalisia pepe itawasaidia wanafunzina kuongeza uwezo wao wa kujifunza kwa vitendo na kuongeza kuwa vifaa hivyo vitakuwa chachu ya mapinduzi katika elimu ya ufundi na ufundi stadi kwani vitawawezesha wanafunzi kupata ujuzi wa kisasa.

Ametaja Shule zilizopokea vifaa hivyo kuwa ni pamoja na Shule ya Sekondari ya Ufundi Iyunga, Shule ya Sekondari ya Ufundi Mfala, Shule ya Sekondari ya Ufundi Nzari na zingine.

Vifaa vilivyotolewa vinajumuisha mashine za VR, kompyuta, kebo za HDMI 330, HPE Aruba Network Access Points 35, Cisco Wireless Access Points 15, seva 10, printa 10, projectors 24, simu janja 40, televisheni janja 3 zenye ukubwa wa inchi 85, pamoja na vifaa vya kusikilizia (headsets) 300.

Aidha, kebo za umeme na vioozi vya mtandao pia vimetolewa ili kuhakikisha vifaa vyote vinaunganishwa katika mtandao na hivyo kufanya kazi kwa ufanisi.

