
Tanzania na Afrika Kusini zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu kufuatia mikutano ya pande mbili iliyofanyika jijini Cape Town.

Mazungumzo hayo yamefanyika Machi 24 jIjini Cape Town Afrika Kusini kati Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Tanzania, Mheshimiwa Wanu Hafidh Ameir, Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu wa Afrika Kusini, Dkt. Nomalungelo Gina, pamoja na Naibu Waziri wa Elimu ya Msingi wa Afrika Kusini, Dkt. Makgabo Reginah Mhaule.

Katika mazungumzo hayo, pande zote zilikubaliana kuimarisha ushirikiano katika tafiti, kubadilishana wanafunzi na watafiti, pamoja na kuendeleza uhusiano kati ya vyuo vikuu na taasisi za utafiti.

Afrika Kusini pia imeeleza utayari wake wa kuendelea kushirikiana na ufadhili wa wanafunzi 16 wa Tanzania wanaosoma Chuo Kikuu cha Johannesburg kupitia mpango wa Samia Scholarship Extended.

Kwa upande wa elimu ya msingi, Dkt. Mhaule alieleza kuwa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili umeendelea kuzaa matunda, hasa kupitia kuimarishwa kwa ufundishaji wa Kiswahili, ubunifu wa mitaala na maendeleo ya walimu nchini Afrika Kusini.

Ziara hiyo imefungua fursa mpya za ushirikiano katika maendeleo ya rasilimali watu, elimu ya kisasa, na uchumi wa maarifa barani Afrika.


