Waratibu elimu kata na wakuu wa shule za msingi na sekondari wametakiwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mwongozo wa urejeaji wa wanafunzi waliokatisha masomo pamoja na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023), ili kuhakikisha hakuna mtoto anayebaki nje ya mfumo wa elimu.



Kauli hiyo imetolewa mkoani Morogoro, Februari 12, 2023 na Patrick Leyana, Mkurugenzi Msaidizi wa Usajili wa Shule, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, alipokuwa akifungua mafunzo kwa niaba ya Kamishna wa Elimu, Dkt. Lyabwene M. Mtahabwa.



Leyana amesema maboresho ya sera hiyo yanalenga kuifanya elimu iwe jumuishi na rafiki kwa wanafunzi wote, huku yakitoa fursa ya pili kwa waliokatisha masomo kurejea na kuendelea na elimu.



Ameongeza kuwa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la Novemba 24, 2021 la kuruhusu wanafunzi waliokatisha masomo kurejea shuleni limefungua fursa kwa makundi mbalimbali, ikiwemo wasichana waliopata ujauzito na watoto waliokumbwa na changamoto za kijamii.



Aidha, amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuimarisha uhamasishaji kwa jamii, kujenga mazingira salama shuleni na kufuatilia maendeleo ya wanafunzi wanaorejea.