
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuboresha elimu nchini kwa kuzingatia mahitaji ya karne ya 21.

Akizungumza Machi 30, 2026 Jijini Dodoma katika hafla ya ugawaji vifaa vya kidijitali, Prof. Nombo amesema kuwa lengo la pamoja kati ya Serikali na Wadau ni kuendeleza elimu na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika mfumo wa ufundishaji na ujifunzaji.

Prof. Nombo ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa matumizi ya teknolojia za kidijitali katika elimu, hatua inayolenga kuimarisha ubora wa ufundishaji na ujifunzaji kuanzia ngazi ya Msingi hadi Sekondari.

Amesisitiza kuwa ugawaji wa vifaa vya kidijitali ni ushahidi wa dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha walimu na wanafunzi wanapata nyenzo bora zinazowawezesha kupata ujuzi wa kidijitali unaohitajika katika dunia ya sasa.

Aidha, Prof. Nombo ameeleza kuwa vifaa hivyo vitachangia kuongeza ufanisi wa elimu na kuandaa kizazi chenye uwezo wa kushindana kimataifa huku akisisitiza umuhimu wa kudumisha usawa kati ya matumizi ya teknolojia na mbinu za jadi kama vitabu na madaftari, ili wanafunzi waendelee kupata ujuzi wa msingi sambamba na ujuzi wa kidijitali.

"Tupo kwenye mapinduzi ya Sayansi na Teknolojia, jamii haitakubali kubaki nyuma katika maendeleo haya. Ugawaji wa vifaa hivi ni hatua muhimu katika kuimarisha elimu bora na endelevu" amesema Prof. Nombo


