Serikali imesisitiza umuhimu wa kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa somo la Hisabati nchini, ikieleza kuwa somo hilo ni msingi wa maendeleo ya sayansi, teknolojia na uchumi wa taifa.



Hayo yameelezwa Machi 13, 2026 jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, wakati akifunga kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Hisabati Dunian akisisitiza kuwa hisabati ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa Sera ya Elimu ya 2014, Toleo la 2023 na mtaala ulioboreshwa, unaolenga kuwajengea wahitimu ujuzi wa kujiajiri na kuchangia maendeleo ya taifa.



Amesema Serikali inaendelea kuimarisha elimu ya sayansi na teknolojia, ambapo Hisabati imebeba nafasi muhimu katika kuwajengea wanafunzi uwezo wa kufikiri, kutatua changamoto na kubuni suluhisho katika maisha ya kila siku.



Aidha, amekipongeza Chama cha Hisabati Tanzania (MAT/CHAHITA) kwa juhudi zake za kuhamasisha ufundishaji na ujifunzaji wa somo hilo, mafunzo kwa walimu pamoja na mashindano ya wanafunzi ya Tanzania Mathematics Olympiads (TAMO). Amesema juhudi hizo zimechangia kuibua hamasa na kuboresha ufaulu wa somo la Hisabati.



Kwa mujibu wa Prof. Mushi, mpango wa walimu kujitolea kufundisha Hisabati katika shule zenye ufaulu hafifu umeonyesha matokeo chanya, ambapo baadhi ya shule za Dar es Salaam zikiwemo Mbopo, Nyeburu na Furaha zimeonyesha kuimarika kwa matokeo ya mitihani ya kidato cha nne katika miaka ya hivi karibuni.



Ameongeza kuwa, ushirikiano kati ya vyuo vikuu na shule umeanza kuzaa matunda, akitolea mfano wa mpango wa mafunzo kwa vitendo kwa walimu wa sayansi na Hisabati ulioanzishwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika shule jirani.