
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Wanu Hafidh Ameir (Mb), ameongoza ujumbe wa Tanzania katika ziara katika Chuo Kikuu cha Johannesburg nchini Afrika Kusini yenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa kielimu kati ya vyuo vya Tanzania na nchi hiyo.

Ujumbe huo umepokelewa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, anayeshughulikia Utafiti na Uvumbuzi Prof. Refilwe Phaswana-Mafuya. Ziara hiyo imewezesha kuimarisha uhusiano wa kielimu na kisayansi baina ya nchi hizo mbili na kufungua majadiliano ya kuanzisha kozi za ufundishaji wa lugha ya kiswahili katika Chuo hicho.

Katika ziara hiyo Mhe. Wanu amekutana na Wanafunzi 16 wa Kitanzania wanaosomea Shahada za Kwanza za Masomo ya Kompyuta; Akili Mnemba (AI); Sayansi ya Takwimu na Tahsusi nyingine za Sayansi na Teknolojia.

Naibu Waziri huyo ameambata na Balozi wa Tanzania nchini humo Mhe. James G. Bwana, Viongozi na Waratibu wa Samia Scholarship Extended (SSE) na Maafisa Waandamizi kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela ( NM-AIST) na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).


