Serikali inaendelea na hatua za kuimarisha huduma za maji safi na mazingira katika shule zote nchini kupitia mpango maalum wa kisekta.



Katika kuwezesha hilo Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amekutana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Bi. Rose Zacharia, Machi 30, 2026 jijini Dodoma kujadili rasimu ya Mpango huo ambao utaiwezesha mazingira bora ya ujifunzaji na ufundishaji.



Katika kikao hicho kilichowashirikisha pia Naibu Katibu Mkuu Elimu Dkt Hussein Omari pamoja na wataalamu kutoka Wizara hizo mbili, walijadili mikakati mahsusi ya utekelezaji, ikiwemo vigezo vya Mradi wa _WASH Compact_ ili kuhakikisha mpango unakuwa wa viwango vya juu na wenye matokeo chanya.



Prof. Nombo alisisitiza umuhimu wa uratibu madhubuti na matumizi sahihi ya rasilimali ili kuhakikisha maandalizi yanakuwa yenye tija na yanayotekelezeka kwa ufanisi.


Rasimu ya mpango huo inalenga kuweka msingi imara wa upatikanaji wa huduma bora za maji safi na mazingira shuleni, huku ukizingatia usawa kwa wanafunzi wote.



Aidha, Utekelezaji wake unatarajiwa kuboresha afya na ustawi wa wanafunzi, kuongeza mahudhurio shuleni, na hatimaye kuinua ubora wa elimu nchini kwa kuchangia mazingira rafiki na salama ya kujifunzia.