
Serikali kwa kushirikian na wadau inaendelea kuimarisha juhudi za kukuza elimu ya vitendo kupitia programu za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM), ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza ubora wa ufundishaji na umahiri wa wanafunzi katika fani za sayansi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, Machi 30, 2026 Jijini Dodoma amepokea taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa STEM kutoka Taasisi ya ProjeKt Inspire ya kipindi cha mwaka 2025 hadi Februari 2026.

Taarifa hiyo imeonyesha mafanikio ikiwemo kuwafikia wanafunzi 15,251 na walimu 456 katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Songwe na Tanga, kupitia programu za mafunzo, ubunifu na uhamasishaji wa ushiriki wa wanafunzi katika masomo ya sayansi.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Prof. Nombo ameipongeza ProjeKt Inspire kwa mchango wake katika kuimarisha elimu ya sayansi nchini na kusisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa elimu ni muhimu katika kuongeza ubora wa mazingira ya kujifunzia na kufundishia, hususan katika masomo ya STEM

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa ProjeKt Inspire, Dkt. Lwidiko Edward, ameeleza dhamira ya taasisi hiyo kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kupitia upanuzi wa vituo vya ubunifu katika shule, kuimarisha mafunzo kwa walimu na kuongeza ushiriki wa wanafunzi, hasa wasichana katika masomo ya sayansi na teknolojia.



