Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga ameahidi kushughulikia changamoto za kielimu zinazoikabili Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga ikiwemo kuanzisha Shule za kidato cha tano na sita na kujenga tawi la Chuo Kikuu cha Mzumbe Mkoani Tanga.



Kipanga amesema hayo katika tukio la Mwalimu Conference 2024 lililofanyika katika Wilaya ya Muheza ambapo alikua Mgeni rasmi kuelekea kilele cha Juma la Elimu Wilayani humo ambacho Mgeni rasmi wake ni Naibu Waziri Mkuu, Dotto Biteko.



Kwa upande wake Naibu waziri wa wa Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Muheza, Hamis Mwinjuma (Mwana FA) amemuomba Mgeni rasmi kusaidia ongezeko la Shule za kidato cha tano na sita katika Wilaya hiyo.



Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Zainabu Abdallah katika Juma la Elimu Wilayani humo lenye kampeni ya 'Mtoto wa leo, Samia wa kesho' wameweza kufika kwenye jumla ya kata sita zenye Shule zaidi ya 12 ili kuwaelimisha Wanafunzi dhamira ya kampeni hiyo ambayo imelenga jinsia zote za Wanafunzi ambapo wanaamini Mtoto Leo anaweza kuja kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania