Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora wa Shule Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ephraim Simbeye, amewataka Maafisa Elimu nchini kutumia kikamilifu teknolojia katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku katika utoaji wa elimu bora.



Ametoa rai hiyo Septemba 18, 2025, mkoani Katavi akizungumza katika Kongamano la Juma la Elimu ya Watu Wazima, ambapo amesisitiza kuwa Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya ndio wasimamizi na watekelezaji wa miongozo ya mitaala ya Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi.



Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuweka mikakati kabambe ili kupandisha kiwango cha elimu ya mfumo huo, ikiwa ni pamoja na kutokomeza tatizo la kutojua kusoma, kuandika na kuhesabu.



Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Watu Wazima kutoka Ofisi ya Rais–TAMISEMI, Mwalimu Ernest Hinju, amesema kuwa kongamano hilo limewaleta pamoja zaidi ya Maafisa Elimu 800 kutoka mikoa yote ya Tanzania, kwa lengo la kujadiliana juu ya njia bora za kuboresha elimu ya watu wazima na kuhakikisha elimu hiyo inakuwa jumuishi, endelevu na yenye tija kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.



Akikabidhi miongozo ya Programu ya Mpango wa Uwiano kati ya Elimu na Jamii (MUKEJA) iliyotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili, Mkurugenzi wa Shirika la Kimataifa la DVV, Frauke Heinze, amesema wanajivunia kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha elimu ya mfumo huo na kwamba elimu ni msingi wa mabadiliko chanya ya kijamii na kiuchumi, na teknolojia ni daraja muhimu kufikia malengo hayo.