Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Nombo leo Oktoba 12, 2023 jijini Dar es Salaam amekutana na kufanya mazungumzo na Bi. Helen Fytche, Kansela Mkuu wa Ushirikiano na Maendeleo kutoka ubalozi wa Canada hapa nchini ambae ameambatana na Bi. Rasmata Barry, muambata wa masuala ya maendeleo ya elimu.

Mazungumzo yamelenga kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Canada na kuona namna ya kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano katika Sekta ya elimu.

Akizungumza katika kikao hicho Prof Nombo amemweleza Bi. Helen kuwa Wizara iko katika hatua za maboresho ya mitaala ya elimu ambayo inajikita katika kujenga ujuzi.

Ametumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali ya Canada kwa ufadhili kupitia miradi ya TESP na UTC na ESP na ameiomba Canada kupitia Ubalozi wake kuendelea kusaidia katika maeneo mapya kama vile ufundi, Ufundi stadi, uwekezaji katika TEHAMA, mafunzo ya uendelezaji taaluma kwa walimu hasa wa ufundi.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Prof. James Mdoe ameongelea uhitaji mkubwa wa kuendelea kutoa mafunzo kwa walimu wa ufundi ili kuwezesha utekelezaji wa mtaala mpya katika hatua za awali za kuanza utekelezaji wake.

Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa ameongezea umuhimu wa kuendelea kupanua wigo wa kusaidia kuendeleza mafunzo katika masomo ya lugha yakiwemo kiingereza na kifaransa