Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa Serikali ipo tayari kukaa na wadau wa Habari ili kupata maoni juu ya uboreshaji mitaala ya mafunzo ya uandishi wa habari.
Akizungumza Novemba 01, 2024 Mkoani Singida katika Mkutano wa Mwaka wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) amesema kuwa lengo la kufanya mapitio hayo ni kuwezesha mafunzo ya uandishi wa habari yaweze kuendana na mabadiliko ya teknolojia.
Prof. Mkenda ameongeza kuwa katika kipindi hiki cha Teknolojia uandishi wa habari nao umebadilika, hivyo hakuna budi kuhakikisha hata mafunzo yanayotolewa vyuoni yanaendana na wakati uliopo.
"Katika maendeleo ya teknolojia kila kitu kimebadilika hivi sasa habari hazitolewi kama kama zamani mambo yote yanakwenda kidijitali, hivyo na mitaala inapaswa kubadilika" amesema Prof. Mkenda
Aidha, Waziri huyo amewataka waandishi wa habari kuendelea kufanya kazi kwa weledi ili kuhakikisha kalamu zao zinaleta tija na kuchochea maendeleo huku akipongeza kazi kubwa wanayofanya kuhabrisha umma.
Prof. Mkenda amewaambia waandishi hao kuwa wao ni macho, masikio, mdomo na ubongo wanaosaidia kuona na kusemea chochote katika jamii kutoa elimu na kusaidia serikali kupata taarifa zinazopelekea kurekebisha maeneo yenye changamoto.
Katika Mkutano huo Waziri Mkenda huyo alipata fursa ya kuelezea mabadiliko ya mitaala na mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 yaliyofanywa na serikali na kuahidi kuendelea kushirikiana na wanahabari katika kutoa elimu kwa umma juu ya mageuzi makubwa yaliyofanyika katika Sekta ya elimu chini ya Serikali ya Awamu ya Sita.