Na WyEST
Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesaini makubaliano na Vyuo na Taasisi za Canada ya kutekeleza Mpango wa Uwezeshaji kupitia Ujuzi (ESP) wenye thamani ya takribani shilingi Bilioni 45.

Hayo yamesemwa Oktoba 26, 2023 Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga wakati akimwakilisha Waziri Prof. Adolf Mkenda katika hafla ya makabidhiano ya Vifaa vya TEHAMA vya kufundishia na kujifunzia kutoka Serikali ya Canada vilivyotolewa kupitia Mradi wa ESP.



Mhe. Kipanga amesema Mradi huo wa miaka saba unaotekelezwa katika vyuo 12 vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) unatarajiwa kunufaisha takribani wananchi 6,776 katika jamii inayozunguka vyuo hivyo ambapo walengwa wa moja kwa moja ni pamoja na wafanyakazi 180, wanafunzi 3,200 na wasichana waliobalehe 720 ambao watapata mafunzo ya ujuzi na jinsia.



“Serikali itahakikisha inatumia kikamilifu msaada huu katika kujenga uwezo wa vyuo 12 vya Maendeleo ya Wananchi ambavyo vipo katika program kwa kuwekeza katika kukuza ujuzi kwa wanawake, vijana na wasichana ili waweze kujikwamua kiuchumi kupitia mafunzo yanayotolewa katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi” amesema Naibu Waziri.



Naibu Waziri ameongeza kuwa lengo la serikali ni kuwa na kompyuta na projekta moja kwa kila darasa ili kumuwezesha mwalimu kufundisha kwa kutumia teknolojia badala ya chaki na kuandaa masomo kwa kutumia Kompyuta hivyo uwepo wa vifaa hivyo utasaidia kujifunza teknolojia za kisasa zilizopo katika soko la ajira.

Akiongea katika makabidhiano hayo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema Mradi wa Uwezeshaji Kupitia Ujuzi (ESP) umejikita katika kuboresha ushiriki wa wanawake na wasichana kujitambua, kufahamu haki zao, kupata ujuzi, kujiinua kiuchumi ili kuchangia katika uchumi wa nchi.