Watekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) leo Oktoba 22, 2024 wamekutana Mkoani Mwanza kufanya mapitio ya utekelezaji wa mradi (Midterm Hb Review) kutathimini mafanikio, kubaini changamoto na maboresho yanayotakiwa kufanyika ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji ili kufikia katika kuleta mapinduzi ya kiuchumi kulingana na malengo ya mradi.



Akizungumza katika kikao hicho cha siku tatu Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Peter Msofe amesema kuwa mkutano huo utapitia taarifa ya kila Taasisi inayotekeleza Mradi ili kufahamu changamoto zilizopo na kuzijadili ili kuzitafutia ufumbuzi wa pamoja.



" Lengo letu ni kuhakikisha Mradi unatekelezwa kikamilifu na kukamilika kwa ufanisi kwa manufaa ya Taifa. Mradi huu utaongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya juu pamoja na kusaidia kuwa na fani zinazoendana na wakati ili kuwasaidia vijana kushiriki katika kujenga uchumi wa Nchi" amesisitiza Prof. Msofe.



Naye Kiongozi wa Timu ya Benki ya Dunia Prof. Roberta Basset Malee amesema lengo la timu hiyo ni kusikiliza taarifa hiyo na kama kuna changamoto ambazo zitahitaji kubadili baadhi ya muundo wa maeneo ya mradi ili waweze kushauri.



Timu ya Benki ya Dunia itatembelea baadhi ya miradi inayotekelezwa katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu ili kujionea utekelezaji wake.