Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amewataka wadau kuiunga mkono Serikali kutekeleza mageuzi ya elimu nchini ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika elimu ujuzi inayolenga kuliwezesha taifa kuwa na rasilimali watu yenye umahiri katika sekta mbalimbali.



Waziri Mkenda ametoa rai hiyo Novemba 14, 2024 jijini Dar es Salaam akifunga Kongamano la Nne la Kimataifa kuhusu ubora wa Elimu, ambapo amesisitiza ni lazima kufanya uwekezaji wa kutosha katika elimu kwa sababu nchi inahitaji rasilimali mahiri itakayochangia maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.



"Naomba wadau tushirikiane kusimamia agenda yetu, tusiondoke kwenye reli, tuwe na mwelekeo mmoja tuwekeze kwenye elimu ujuzi ili kuhakikisha watoto na vijana wetu wanapata elimu bora na yenye ujuzi" Alisema Mkenda.



Aidha Prof. Mkenda amewaeleza wadau hao kuwa katika mfumo mpya, elimu ya lazima itakuwa ni miaka 10, ambapo baada ya elimu ya awali ,unaanza elimu ya msingi miaka sita, elimu ya chini ya sekondari miaka minne. Aidha elimu ya Sekondari ya juu ni miaka miwili.



Akizungumza kuhusu kongamano hilo lililoongozwa na kauli Mbiu , kukuza mifumo imara ya elimu kwa maendeleo endelevu barani afrika, Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa Elimu Tanzania Bi. Martha Makala amesema kuwa wadau hao wamekuwa mstari wa mbele katika kuchangia sekta ya elimu kuwezesha nchi hizo kuendana na mabadiliko ya kielimu na kisera.



‘’Tunatambua Tanzania tumepitia kwenye mageuzi makubwa ya kisera na kimitaala, tutaendelea kuiunga mkono Serikali katika kutekeleza mageuzi hayo, kwa kuzingatia kuwa elimu ujuzi itawawezesha wanafunzi kutumia rasilimali zilizopo kwenye maeneo yao kujiajiri na kuchangia pato la taifa’' alisema Bi. Makala.

Amezitaka nchi za Afrika ziindelee kuimarisha na kuboresha mifumo ya kuwabakiza shule wanafunzi wanaoonekana kuwa na viashiria vya mdondoko ili kubaki shule waweze kukamilisha mzunguko wa masomo yao