Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Tanzania Bara kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar wameendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta ya elimu, kwa lengo la kuhakikisha mfumo wa elimu unakidhi mahitaji ya soko la ajira la kitaifa, kikanda na kimataifa.



Akizungumza Agosti 21, 2025 Jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, alieleza kuwa ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar ni hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa elimu na kuongeza tija kwa jamii.



Kikao hicho kimetoa fursa ya kujadili mafanikio yaliyopatikana, changamoto zinazojitokeza, na fursa zilizopo, huku viongozi wakikubaliana kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma bora za elimu.



Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Bw. Khamis Abdulla, alieleza kuwa ushirikiano huo ni chachu ya maendeleo ya elimu nchini. Alibainisha kuwa kupitia programu za WYEST na WEMA Zanzibar, Serikali zote mbili zinaendelea kushirikiana katika kuboresha mitaala, kuongeza uwezo wa walimu, na kujenga mazingira bora ya kujifunzia.



Matarajiwa ya ushirikiano huo ni kuwa na mikakati madhubuti ya kuimarisha ubora wa elimu, kuongeza ushirikiano wa kitaasisi, na kuimarisha mchango wa sekta ya elimu katika kukuza uchumi wa taifa na maendeleo ya kijamii. Kikao hicho kimejumuisha viongozi na watumishi kutoka Wizara za Elimu Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na taasisi zake