
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, amewataka Watanzania hususan vijana kutomtazama Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kama historia tu, bali kama msingi imara na Dira ya Maendeleo ya Taifa.

Akizungumza katika Kongamano la 12 la Kumbukizi ya Kuzaliwa kwa Mwalimu Nyerere lililofanyika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Kampasi ya Kivukoni, Prof. Mushi amesema falsafa ya Mwalimu katika kujenga amani na mshikamano wa kitaifa ni kielelezo cha uzalendo na upendo na kusisitiza kuwa mshikamano uliopo nchini ni matokeo ya misingi aliyoipanda Baba wa Taifa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Ndg. Stephen Masato Wasira, amesema falsafa ya Mwalimu imesimama katika misingi minne: Uhuru, Umoja, Maendeleo na Ukombozi wa Afrika na kueleza kuwa misingi hiyo bado ni muhimu katika dunia ya sasa.

Mzee Wasira aliwataka vijana kutambua kuwa amani na umoja si bahati mbaya, bali ni zao la falsafa imara za uongozi. Amesisitiza wajibu wa vijana kuelewa falsafa hizo ili wawe viongozi bora wa baadaye.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Prof. Haruni J. Mapesa, alieleza mafanikio ya taasisi hiyo. Ametaja ongezeko la udahili kufikia wanafunzi 16,150 kwa mwaka wa masomo 2025/26, maboresho ya mifumo ya TEHAMA na miundombinu ya kufundishia.

Kongamano hilo liliongozwa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bi. Anne Makinda. Mada kuu ilikuwa Falsafa ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika Kujenga Amani na Mshikamano wa Kitaifa Tanzania, ikichagizwa na mada ndogo kuhusu Umoja wa Kitaifa na Mshikamano wa Kijamii.


