Ufunguzi wa kiwanda cha Federal Industry Limited kilichopo Mkuranga mkoani Pwani unatarajiwa kuongeza ajira kwa wananchi, kukuza uzalishaji na kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa.



Akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi huo Machi 17, 2026, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wannnu Hafidh Ameir, amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kujenga uchumi wa viwanda.



Ameeleza kuwa Serikali, kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya elimu, inaendelea kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi na maarifa yanayokidhi mahitaji ya soko la ajira, hususan katika sekta ya viwanda.



Aidha, amefafanua kuwa tarehe 9 Februari 2026 Serikali ilizindua Mkakati wa Kitaifa wa Ushirikiano kati ya taasisi za elimu na mafunzo, viwanda pamoja na waajiri, kwa lengo la kukuza ujuzi unaohitajika na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.



Ametoa wito kwa wamiliki wa viwanda na waajiri kuendelea kushirikiana na taasisi za elimu na mafunzo kwa kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo na kushiriki katika uandaaji wa mitaala ili kuandaa rasilimali watu wenye umahiri na kuongeza tija ya uzalishaji.



Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tiantang Group na mwekezaji wa Federal Industry Limited, Bw. Paul Zhang, amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa kukuza sekta ya viwanda Afrika Mashariki, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wawekezaji wa China na wadau wa ndani katika kujenga uchumi imara.