Serikali kupitia Wizara ya Elimu inatarajia kutumia Sh. Bilioni 6 kutoa ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa mwaka 2023/24 kupitia Mpango wa Samia Scholarship kwa wahitimu wa kidato cha Sita wapatao 640.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesisitiza ufadhili huo utagharamia elimu ya juu kwa asilimia 100 kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza waliopata ufaulu wa juu katika Mitihani ya Kidato cha Sita mwaka 2023 inayoendeshwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) katika tahasusi za Sayansi na kuchaguliwa kujiunga na Programu za Sayansi Teknolojia, Elimu Tiba na Hesabu katika Vyuo vikuu nchini.

Ameeleza kuwa Maombi ya Samia Scholarship yatawasilishwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa https://olas.heslb.go.tz kuanzia Jumatatu, Septemba 25, 2023.

Amesisitiza kuwa Skolashipu hizo zitaendelea kutolewa kwa haki na kwa uwazi , kwani vigezo vinafahamika na vitafuatwa na kwamba lengo ni kuongeza chachu ma idadi ya wanasayansi nchini.

“Samia Skolashipu inalenga kuongeza idadi ya wanasayansi nchini ambao watachangia moja kwa moja katika maendeleo ” amesisitiza Waziri huyo.

Amesema Idadi ya wanafunzi watakaokuwa wamefadhiliwa na Scholarship hiyo katika miaka miwili itakuwa imefikia wanafunzi 1276.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa ufadhili utazingatia viwango na miongozo ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu na utagharamia maeneo ya ada ya mafunzo, posho ya chakula na malazi, Vitabu na Viandikwa, utafiti, Bima ya Afya, mahitaji maalum ya vitivo, mafunzo kwa vitendo na vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na kwamba Orodha ya majina ya wanafunzi wenye sifa za kuomba itapatikana kupitia www.moe.go.tz na www.heslb.go.tz kuanzia wiki ya kwanza ya mwezi Agosti, 2023.

Prof. Nombo amesisitiza kuwa Mwanafunzi atakaepata ufadhili wa SAMIA SCHOLARSHIP atapaswa kuzingatia masharti ambayo ni pamoja na Kusoma, kuelewa na kusaini Mkataba wa Makubaliano ya Ufadhili wa Masomo kati yake na Wizara ya Elimu.