Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amefunga Mkutano wa 37 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo kwa kusisitiza umuhimu wa ushirikiano, uwajibikaji na utekelezaji wa maelekezo ya Serikali katika kuimarisha sekta ya elimu.



Akizungumza Aprili 30, 2026 Jijini Dodoma, Naibu Waziri ameeleza kuwa mageuzi yanayoendelea katika elimu yanatokana na dira thabiti ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.



Naibu Waziri amebainisha kuwa hatua muhimu zinazotekelezwa na Serikali, ikiwemo Mkakati wa Kisayansi wa Kuimarisha Stadi za KKK uliozinduliwa pamoja na Mpango wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Waajiri inalenga kuboresha ufundishaji, kuongeza ubora wa wahitimu na kuimarisha uhusiano kati ya nadharia na vitendo ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira.



Aidha, Naibu Waziri ameongeza kuwa maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 toleo la 2023 pamoja na kuhuishwa kwa mitaala ni hatua muhimu zinazowezesha vijana kupata maarifa na umahiri unaohitajika katika uchumi wa kisasa unaoongozwa na sayansi na teknolojia.



Ameipongeza Menejimenti ya Wizara na wajumbe wa Baraza kwa kuendelea kusimamia majukumu kwa weledi na kuimarisha utawala bora.



Naibu Waziri amewataka watumishi kuendelea kudumisha nidhamu, mshikamano na uadilifu, sambamba na kutekeleza kwa vitendo maelekezo yaliyotolewa na Waziri wakati wa ufunguzi wa mkutano.



Amesisitiza umuhimu wa ufuatiliaji, tathmini endelevu na ushirikiano kati ya Wizara, taasisi zake, TAMISEMI na wadau wa elimu katika kutekeleza sera ya elimu ya lazima ya miaka 10.