Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa wito wa kujiandaa na mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea duniani, akisisitiza kuwa ajira za sasa na zijazo zinahitaji ujuzi, maarifa na matumizi ya teknolojia mpya.



Akizungumza katika Maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi, 2026) mkoani Njombe Mhe Rais amebainisha kuwa bila kuwekeza katika maeneo hayo, nguvu kazi ya taifa haitakuwa na uwezo wa kukabiliana na ushindani wa kimataifa.



Ameongeza kuwa, jukumu hilo linapaswa kubebwa kwa pamoja na Serikali na sekta binafsi kwa kuwekeza kwa makusudi katika elimu na ukuzaji wa ujuzi ili kuijenga nguvu kazi yenye uwezo wa kuhimili mabadiliko ya soko la ajira na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi.



Aidha, Rais Samia amesema Serikali itaendelea kurasimisha sekta isiyorasmi ambayo inaajiri mamilioni ya Watanzania, ili kuongeza tija na ulinzi wa wafanyakazi.