
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Anneth Komba ameeleza kuwa uandishi bunifu ni nyenzo muhimu ya kufanikisha malengo ya elimu nchini.

Akizungumza Aprili 13, 2026, katika hafla ya utoaji Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu amesema kuwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la 2023 inalenga kuandaa wanafunzi wenye stadi ikiwemo za kusoma,, kuandika na kuwasiliana kwa lugha Kiswahili kwa ufasaha, na kutambua tamaduni za Kitanzania.

Aidha, ameongeza kuwa uandishi bunifu ni chombo cha kujenga fikra makini, uwezo wa kuchambua na kutatua changamoto mbalimbali huku ukilinda misingi ya umoja wa kitaifa na maadili ya jamii yetu.

Akizungumzia nafasi ya fasihi ya Kiswahili, Mkurugenzi Mkuu huyo amebainisha kuwa somo hilo ni daraja la kukuza uandishi bunifu kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari.
Ameongeza kuwa Fasihi huwapa wanafunzi uwezo wa kutunga mashairi, tamthiliya, hadithi na riwaya, na pia huendeleza stadi za kushawishi na kujenga hoja na kupitia uandishi bunifu, wanafunzi hujengewa ukamilifu wa fikra, kujiamini na umahiri wa kutumia stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (3R), hivyo kuimarisha uwezo wao wa kitaaluma na kijamii.

Dkt Komba amesisitiza kuwa Fasihi ya Kiswahili imekuwa chachu ya kuendeleza ubunifu na kuimarisha utamaduni wa kusoma na kuandika na kwamba mchango wa “Tuzo” ni kuimarisha uandishi bunifu na fasihi ya Kiswahili na kuongeza hazina ya vitabu vya fasihi, kuimarisha uchambuzi wa lugha na kukuza ubunifu miongoni mwa wanafunzi.


