Katika kuendelea kuimarisha juhudi za kuhakikisha wanafunzi wanapata lishe bora wakiwa shuleni, Shirika la Chakula Duniani (WFP) wameahidi kuendeleza ushirikiano na Serikali katika eneo hilo.



Hayo yameelezwa tarehe 9 Machi, 2026 jijini Dodoma na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP), Bw. Ronald Tran Ba Huy, alipokutana na Waziri wa Elimu, Sayandi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ambapo amesema WFP imejizatiti katika kuendelea kufadhili programu za Chakula Shuleni, ili kuhakikisha lishe inachangia kuongeza mahudhurio ya wanafunzi, kuimarisha ustawi wao na kuongeza ufaulu.



WFP inafadhili programu hiyo katika mikoa miwili ya Lindi na Mtwara ambapo imeonesha mafanikio kwa kuongeza ufaulu kwa asilimia 9 na wameahidi kupanua wigo kwa kuongeza mikoa mingine pamoja na kushirikiana katika kuwekeza nishati safi ya kupikia katika shule na vyuo vya kati.



Kwa upande wake Prof. Mkenda amepongeza hatua hiyo na kuwaeleza kuwa serikali inaipa umuhimu suala la chakula salama shule na kuwa inakuja na mpango wa pamoja kati ya Wizara ya Elimu, Waziri Mkuu TAMISEMI na Wizara ya Kilimo ili kuwa na mpango endelevu.