
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa uzinduzi wa Mpango wa Kitaifa wenye lengo la Kukuza Ujuzi na Ajira ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati wa Kampeni za uchaguzi kwa mwaka 2025 kwamba ndani ya siku 100 endapo atachaguliwa na kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Serikali ingeandaa na kuzindua Mpango wa kukuza ujuzi na uwezo wa kuajirika kwa vijana, na sasa ahadi hiyo imetimia kabla ya muda uliowekwa.

Prof. Mkenda ameeleza kuwa Mpango huu umeandaliwa kwa kushirikisha na wadau mbalimbali ikiwemo Vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Waajiri na Wataalamu waliobobea katika kuboresha mitaala na kuongeza ujuzi akisisitiza kuwa ushirikiano huu ni msingi wa kuhakikisha Wahitimu wanapata ujuzi stahiki unaohitajika katika soko la ajira

"Yapo mafanikio tumeanza kuyaona ya ushirikino na viwanda, Wahitimu wa VETA, hususan VETA Moshi, wamekuwa wakipata ajira ndani na nje ya nchi katika maeneo kama Namibia, Guinea-Conakry, Mauritania, Kongo na Ghana hivyo uzinduzi huu utahamasisha waajiri kushirikiana zaidi, wazazi kuelewa umuhimu wa kuwapeleka watoto shuleni kupata ujuzi, na hatimaye kuchangia katika kuinua uchumi wa Tanzania," amesisitiza Prof Mkenda.


