
Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imetoa wito kwa halmashauri na wadau mbalimbali kuwekeza katika maeneo zinakojengwa kampasi mpya 16 za vyuo vikuu nchini.

Rai hiyo imetolewa jijini Dodoma Februari 02, 2026 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, katika kikao cha pamoja kati ya watekekeza mradi na wakurugenzi wa Halmashauri.

Prof Mushi amesema halmashauri na serikali za mitaa zina wajibu wa kutenga ardhi na kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi kwa kushirikiana na vyuo vikuu vinavyojenga katika maeneo yao ili kuruhu uwekezaji kwa ajili ya huduma mbalimbali.

Amesisitiza kuwa ni muhimu uwekezaji utakaofanyika uendane na mipango ya miji, usalama na kwa kuzingatia viwango.

Amesema hatua hiyo inalenga kuzuia ujenzi holela na kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi mahitaji ya wanafunzi, watumishi wa vyuo pamoja na jamii zinazozunguka maeneo hayo.

Amesisitiza kuwa ili kufanikisha kunahitajika ushirikiano wa karibu kati ya Wizara Vyuo mikoa na halmashauri katika maeneo hayo zinapojengwa kampasi hizo mpya ambapo pia itasaidia
kuondoa migongano ya matumizi ya ardhi.

Katika hatua ingine Prof. Mushi amebainisha umuhimu wa vyuo vikuu kufungua milango ya ushirikiano na sekta binafsi kupitia ubia rasmi (PPP) katika ujenzi wa hosteli, vituo vya biashara na miundombinu mingine muhimu huku halmashauri zikihakikisha mazingira wezeshi kwa wawekezaji Na kutumia fura hiyo kualika wadau wa sekta binafsi kuwekeza katika maeneo hayo.


