
Mpango wa Kuimarisha na Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) umewezesha upatikanaji vifaa vya TEHAMA katika shule teule na vituo vya walimu 400 ili kurahisisha ujifunzaji na ufundishaji kwa njia za Kisasa kutumia teknolojia.
Kupitia mpango huo walimu 600 wa TEHAMA, walimu wakuu 600 na waratibu elimu kata 450 wamepata mafunzo ya matumizi Bora ya vifaa hivyo vya TEHAMA katika kuleta tija kwenye ufundishaji na ujifunzaji.
Mwalimu wa TEHAMA katika Shule ya Msingi Ramadhani iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Njombe Silivia Mbilinyi, amesema kuwa mafunzo waliyopata yamekuwa chachu ya mabadiliko katika mbinu za kufundishia, na sasa wanafunzi wanashiriki kikamilifu darasani kupitia matumizi ya vifaa vya TEHAMA.
Naye, mwalimu Erasto William kutoka Shule ya Msingi Nyambogo iliyopo katika Halmashauri ya Makambako amesema kuwa walimu wengi wameweza kubuni mbinu bunifu za kufundisha, na hivyo kuifanya elimu kuwa ya kuvutia na ya kisasa zaidi kwa wanafunzi wa shule za msingi.