Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amewataka Watanzania kujivunia kwa maendeleo yaliyopatikana katika sekta mbalimbali zinazogusa wananchi moja kwa moja.
Akizungumza na viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Njombe Septemba 20, 2024 wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali mkoani humo ambapo amesema kuwa wakati nchi inapata uhuru hakukuwa na Chuo Kikuu hata kimoja lakini pia kuanza darasa la saba ilikuwa shida.
Prof. Mkenda ameongeza kuwa mpaka sasa kuna vyuo vikuu, kuna shule za kutosha ambazo zinawezesha watoto wote waliofikia umri wa kwenda shule wanakwenda.
"Lazima tukubali kuwa toka tupate uhuru kuna hatua kubwa imepigwa katika maendeleo ya nchi ambayo yanatuwezesha kupiga kifua na kujidai kwa hatua kubwa iliyopigwa" amesisitiza Prof. Mkenda
Waziri Mkenda amesisitiza kuwa wakati inapata uhuru barabara zilikuwa za vumbi na kwa upande wa elimu miundombinu haikuwa ya kutosha na haikuwa ya kuridhisha lakini kwa sasa katika nchi nzima kuna miradi mbalimbali ya barabara, maji, afya na elimu inatekelezwa kwa kasi kubwa.
Aidha, amewataka watanzania kutambua kuwa serikali inaendelea na uboreshaji wa huduma za jamii na ndo maana katika kipindi cha uongozi wa serikali ya Awamu ya Sita imewekeza kwa kiasi kikubwa katika miundombinu ya elimu, afya, barabara na maji.
"Hatuwezi kukataa kwamba hakuna changamoto, zipo na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano anaendelea kutuekekeza sisi Mawaziri wake kuendelea kuzitatua ili ifike wakati tuzimalize kabisa" ameongeza Mkenda.