Wazira ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, amezindua miongozo minne ya elimu maalum na jumuishi ambayo inalenga kuboresha utoaji wa elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum .

Miongozo hiyo ni pamoja na mwongozo wa shule ya nyumbani, ziara ya nyumbani, upimaji na ubainishaji na uendeshaji wa elimu maalum na jumuishi.

Akizindua miongozo hiyo Septemba 12, 2023 jijini Dodoma, Prof.Mkenda amesema miongozo hiyo italeta mabadiliko chanya miongoni mwa wadau katika kutimiza azma ya Serikali ya kuwapatia fursa ya elimu bora wanafunzi wenye mahitaji maalum nchini.

Ametoa wito kwa viongozi, wakuu wa Taasisi na wadau wanaojishughulisha na utoaji elimu maalum na jumuishi kuendelea kushirikiana na serikali kuhamasisha umuhimu wa elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum.

“Natoa rai kwa familia na wadau wa maendeleo waendelee kuona umuhimu wa kuchangia juhudi za Serikali katika kuwapatia huduma stahiki wanafunzi wenye mahitaji maalum ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa ujifunzaji,”amesema Prof. Mkenda

Amehimiza wazazi kuona umuhimu wa kuandikisha watoto wote wenye mahitaji maalum katika shule kwa kuzingatia mahitaji ya mtoto.

“Kwa wale watakaohitaji huduma hii ipelekwe majumbani basi wawasiliane na sisi ili kuangalia namna tutakavyoweza kufikisha huduma hii nyumbani kwa mtoto,”amesema.

Aidha, amesema katika Rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 toleo la 2023 somo la elimu jumuishi na lugha ya alama litakuwa ni lazima kwa mtu yeyote anayeandaliwa kuwa mwalimu hapa nchini.

“Jitihada hizi kubwa mnazoziona zinatokana na msimamo wa Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan na nyie wote mnajua ni mashahidi maandalizi haya yalianza mapema na kama mnavyofahamu Rais wetu anataka kuhakikisha kila mtoto anakwenda shule,”amesema.

Prof Mkenda ameushukuru Mfuko wa Serikali ya watu wa Uingereza (UKAID) kupitia program ya Shule Bora na  Ali Kimara Foundation kwa kuchangia uandaaji na uchapishaji wa miongozo hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo Kamishna wa Elimu Dkt. Lyabwene Mtahabwa amesema maendeleo yoyote duniani yanaletwa na elimu na kwamba elimu bora inategemea walibu wa nyumbani ambao ni wazazi na walezi, shuleni na mazingira hivyo miongozo iliyozinduliwa inalenga itasaidia katika maeneo hayo

Awali, Mkurugenzi wa Elimu maalum wa Wizara hiyo, Dkt. Magreth Matonya amefafanua kuwa  mwongozo wa Shule ya Nyumbani utasaidia kuhakikisha haachwi nyuma mtoto yeyote kwenye kupata elimu.

Amesema mwongozo wa ziara ya nyumbani unakwenda kuwasaidia walimu wanaokwenda ziara za nyumbani kupata taarifa zitakazowezesha kuchukua hatua stahiki.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Awali na Msingi, kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mwl.  Susana Nussu, amesema  TAMISEMI ipo tayari kuendelea kusimamia na kutekeleza miongozo inayotolewa ya elimu Maalum na Jumuishi na kuhakikisha kwamba watoto wote wenye mahitaji Maalum wanasimamiwa na wanapata elimu na afua stahiki.

Kadhalika, Mzazi wa Ali Kimara ambaye mtoto mwenye ugonjwa adimu, Sharifa Mbarak ameshukuru Serikali kwa kuzindua miongozo hiyo na kwamba ni hatua kubwa zilizopigwa na taifa katika utoaji elimu stahiki  kwa wanafunzi wenye Mahitaji Maalum.