Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo ameitaka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kuwa na mfumo mathubuti wa kuratibu tafiti mfumo ambao utaosomana na Taasisi nyingine za kitafiti.

Ametoa agizo hilo Julai 31, 2023 mjini Morogoro katika Kikao kazi cha kujadili usimamizi wa utafiti na maendeleo nchini ambapo amesema ili kutekeleza hilo kwa ufanisi wizara itaunda kamati ndogo shirikishi ambayo itapitia maoni ya kikao kazi na kuangalia sheria mbalimbali za taasisi zinazohusu masuala ya tafiti ili kutoa mapendekezo.

"Utafiti ni muhimu kwa maendeleo ni vyema ukaratibiwa vizuri ili kupunguza milolongo ya kupatikana kwa vibali vya kufanya kazi hiyo na kuwezesha upatikanaji wa matokeo kwa urahisi" amesisitiza Prof. Nombo.

Katibu Mkuu huyo ameongezea kuwa ni muhimu kwa taasisi kujikita katika kufanya tafiti za pamoja ili kuleta tija katika tafiti zinazofanyika.

Aidha ameshauri Taasisi za kitafiti katika sekta mbalimbali kuhakikisha zinatenga fedha kwa ajili ya kufanya utafiti utakaowezesha kutatua changamoto kuchochea maendeleo.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu Prof. Maulillio Kipanyula amesema kuwa kikao kazi hicho kinafanyika kwa kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ina jukumu la kutunga na kusimamia utekelezaji wa Sheria na Miongozi ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Utafiti.

Naye Mshiriki wa Kikao hicho Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Prof. Lughano Kusiluka ameipongeza wizara kwa kuwaleta wadau pamoja na kushauri kifanyike mara kwa mara ili kujadili vipaumbele, utekelezaji na matokeo ya tafiti katika maendeleo.