Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ameitaka Bodi ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kujiimarisha kutekeleza majukumu yake mahsusi ili kutimiza kiu ya watanzania wanaotaka kusoma elimu bila kikomo na sio kurudufu kazi za taasisi nyingine.

Prof. Mkenda amesema hayo Julai 28, 2023 Jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea Taasisi hiyo na kuzungumza na Bodi na menejimenti ambapo amesisitiza kuwa fursa za kusoma lazima zipatikane katika maisha yote ya binadamu hivyo ili kuendana na mabadiliko mbalimbali Taasisi inapaswa kuangalia upya jinsi ya kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kulingana na wakati.

Kiongozi huyo pia amewataka kushirikiana na wadau mbalimbali wenye uzoefu na uelewa juu ya mifumo ya elimu bila ukomo ili kuangalia ni mambo gani yanapaswa kuongezwa ama kupunguzwa ili kuleta ufanisi na kuongeza tija.

“Kuna Taasisi nyingi ambazo zinatoa elimu bila ukomo za serikali kama Chuo Kikuu Huria na Taasisi nyingine za binafsi hivyo ni muhimu kwa bodi kushirikiana nao ili mpate mbinu mpya badala kufanya kazi ambazo zinafanywa pia na taasisi nyingine” ameongeza Prof. Mkenda

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema Taasisi hiyo inafanya kazi nzuri lakini baada ya matokeo ya sensa yameonyesha kuna asilimia kubwa ya watanzania ambao bado hawana ujuzi wa kusoma na kuandika vizuri hivyo ni kazi ya taasisi hiyo kuhakikisha watanzania wanakuwa na maarifa ya msingi ya kusoma na kuandika.



Prof. Nombo ameongeza kuwa katika kutatua changamoto hiyo ya watu kutokujua kusoma na kuandika, kupitia miradi na programu taasisi hiyo itawezesha kupunguza idadi ya watanzania wasiojua kusoma na kuandika, kwani haiwezekani kufanya maendeleo yeyote bila ya kuwa na ujuzi wa kawaida wa kusoma na kuandika.

“Juzi Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kilele cha mkutano wa viongozi wa Afrika juu ya rasilimali watu alisema Watanzania ambao tunaona kuanzia mtoto mpaka mzee, wote wanapaswa wapate ujuzi wa kusoma na kuandika. Hivyo taasisi yetu hii lazima tuhakikishe tunawatendea haki walengwa hawa kwa kuwapa stadi hizo” amesisitiza Prof. Nombo