Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano qa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amewataka walimu kote nchini pamoja na kazi nzuri wanayoifanya kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kujituma.

Makamu wa Rais ametoa agizo hilo wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma alipokuwa akipokea madarasa 3, ofisi 2 yaliyokarabatiwa na Benki ya Biashara ya Tanzania (TCB) pamoja na ununuzi wa madawati 25, computer na photocopier.

Aidha Mhe. Mpango amewataka Wazazi kupeleka watoto shule na kuhakikisha wanasoma. Amesema Rais amefanya uamuzi wa kijasiri kuondoa ada kuanzia elimu ya Msingi hadi kidato cha sita hivyo watoto wasiachwe nyumbani bila kwenda shule.

"Acheni mabinti wasome wamalize tusiharakishe kuwaoza watoto wadogo, hatutapata madaktari, maprofesa,"amesema Dkt. Mpango

Na kuongeza "Kuanzia mwaka huu kwenye shule hii niliyosoma ya Muyama nitaanzisha tuzo ya mwanafunzi bora atakaepata ufaulu mzuri atapata Sh milioni moja, mwanafunzi bora wa kike milioni moja na mwalimu atakaefaulisha katika masomo anayofundisha vivyohivyo,"amesema Dkt. Mpango.

Amewataka wadau wengine kuiunga mkono Serikali katika kuboresha mazingira ya ufundishaji na kujifunzia hasa katika maeneo ya Vijijini.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Thobias Andengenye amesema Mkoa ulipokea Sh bilioni 53.7 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya elimu pamoja na utoaji wa elimu bila ada.

Ameishukuru Serikali pia kuuletea mkoa huo fedha kwa ajili ya ujenzi wa VETA kila Wilaya, ujenzi wa Chuo cha TIA eneo la Kabanga na kutenga Sh. Bilioni 36 kwa ajili ya kuanza ujenzi Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba tawi la Muhimbili.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Dkt. Franklin Rwezimula ameshiriki katika hafla hiyo iliyofanyi Buhigwe mkoani Kigoma.