WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha masuala ya sayansi, teknolojia na ubunifu yanachochea kasi maendeleo ya uchumi nchini.
Prof.Mkenda ameyasema hayo leo Aprili 28, 2023 jijini Dodoma katika kilele cha Wiki ya Ubunifu kitaifa ambapo amesema sayansi, teknolojia na ubunifu zina mchango mkubwa wa kuchagiza maendeleo ya kiuchumi na kwamba nchi mbalimbali zimefanikiwa kutokana na kuwekeza kwenye eneo hilo.
“Ibara ya 102 ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inaahidi kuwa Serikali itahakikisha inaendeleza sayansi, teknolojia na ubunifu, tunachokifanya hapa leo ni kuendeleza yale ambayo chama chenye Serikali kilitoa ahadi wakati wa kuomba kura kwa wananchi. Baada ya kufanya maonesho haya na MAKISATU tunaona sasa tunapata bidhaa zilizoibuliwa, zimebiasharishwa na ni jukumu letu kuzitangaza,”amesema Prof Mkenda.
Ameongeza “Nchi ya Norway iliendelea kwasababu iliwekeza kwenye elimu hasa sayansi, teknolojia na ubunifu na nchi nyingine nyingi zimeendelea kwasababu hii kuwezesha sayansi na teknolojia na baadae kuziingiza teknolojia zao sokoni, tusidhani suala hili ni dogo wote walioanza na ubunifu walianza kwa kubezwa zamani miaka ya 50 magari ya Japan yalikuwa yakibezwa leo hii barabarani magari mengi ni ya Japan.” ameongeza Prof. Mkenda
Waziri Mkenda ametumia nafasi hiyo kuwashukuru
Wadau mbalimbali walioshiriki katika kuhakikisha wiki ya Ubunifu Tanzania inafanikiwa.
“Niwashukuru wadau mbalimbali ambao wameungana nasi kufanikisha maonesho haya napenda kutoa shukrani za pekee kwa UNDP na wadau wengine kwa kutushika mkono kupitia program ya FUNGUO, benki ya NMB, CRDB, UNESCO, WFP, LM International na TANZTECH ambao wataanza kuzalisha vishikwambi nchini na wataungana na sisi kupitia vyuo mbalimbali ili kusaidia wanafunzi wetu kuingia kwenye mafunzo maalum ya masuala ya kielektroniki na uhandisi,”amesema Prof. Mkenda