Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema mapitio na mabadiliko ya Sera ya Sayansi Teknolojia ya mwaka 1996 yanafanyika ili kuakisi mahitaji na kasi ya mabadiliko ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu nchini.
Prof. Nombo amesema hayo jijini Dodoma wakati akifungua Kikao kazi cha kujadili na kupokea maoni hya wadau juu ya Rasimu ya Sera ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu na Kiunzi cha Uratibu wa masuala ya Ubunifu nchini.
Amesema mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii yanayotokea Duniani yanatokana na kutilia mkazo na kuwekeza kikamilifu kwenye Sayansi, Teknolojia na Ubunifu na ndio maana Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuwekeza katika eneo hilo ili kuongeza kasi ya maendeleo, pato la Taifa na kuboresha maisha ya wananchi.
“Mtaona Serikali inawekeza fedha nyingi kwenye STU hii inatokana na umuhimu wake katika shughuli za kiuchumi na kijamii, nitoe rai kwa watanzania kuendelea kutumia fursa zilizotolewa kutoa maoni ili kuhakikisha tunapata Sera na Kiunzi madhubuti kitakachojibu mahitaji na matarajio ya nchi” amesema Prof. Nombo.
Prof. Nombo ametaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kutokana na utekelezaji wa Sera ya Sayansi na Teknolojia ya mwaka 1996 kuwa ni kuongezeka kwa Taasisi za utafiti na maendeleo kutoka 18 mwaka 1961 hadi kufikia 94 mwaka 2021 na kuanzisha Mfuko wa Taifa wa Uendelezaji wa Sayansi na Teknolojia (MTUSATE).
Pia imesaidia kuzalisha teknolojia mbalimbali zenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi, chanjo mpya za magonjwa ya mifugo, teknolojia rahisi za kusafisha maji ya kunywa na uzalishaji wa mbegu mpya za mazao na wanyama.
Nyingine ni kupandishwa hadhi kwa Chuo cha Ufundi Dar es Salaam kuwa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia Mbeya kuwa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya na kuongezeka kwa idadi ya watafiti kutoka Taasisi za Elimu ya Juu na taasisi za Utafiti na maendeleo ya umma kutoka 3,593 mwaka 2007/08 hadi kufikia 10,966 mwaka 2021.
Nae Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Aloyce Kamamba amesema eneo la sayansi teknolojia na ubunifu linagusa jamii moja kwa moja hivyo kufanyika kwa kikao kazi hicho kinatoa fursa kwa Wizara kuwa na mawanda mapana ya kupata maoni yatakayosaidia kuwahudumia vijana wa kitanzania kupitia bunifu wanazozalisha.
Kwa uapande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya uwekezaji wa Mahitaji ya Umma Jerry Silaa (Mb) ameipongeza Wizara kwa kuitisha Mkutano huo kwa kuwa ni eneo muhimu linaloweza kusaidia kutatua changamo za ajira kwa vijana wa kitanzania.
Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Maulilio Kipanyula amesema na lengo la kikao kazi hicho ni kutoa fursa kwa wadau kujadili na kutoa maoni kwenye rasimu ya Sera na kiunzi cha uratibu wa masuala ya ubunifu ili kuja suluhisho katika kuibua, kutambua na kuendeleza wabunifu na bunifu zinzozalishwa.
Kikao kazi cha kupitia Rasimu ya Sera ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu pamoja na Kiunzi cha masuala ya ubunifi nchini kinafanyika kwa siku mbili na kimehusisha wadau zaidi ya 200 kutoka makundi ya Sekta ya umma na binafsi kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ili kupata wigo mpana kwa wadau wa eneo hilo.