Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, ameonesha kuridhishwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Mloganzila, ambapo hadi kufikia Desemba 2025 utekelezaji wa jumla wa mradi umefikia zaidi ya asilimia 55, na miradi mingi ikiwa iko mbele ya ratiba iliyopangwa.



Prof. Mkenda ametoa kauli hiyo tarehe 17, Desemba, 2025 Mkoani Dar es salaam wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya Ndaki ya Tiba na majengo mengine ya kufundishia na kujifunzia katika kampasi hiyo, akisema mradi huo ni uwekezaji wa kimkakati wa Serikali katika kuimarisha rasilimali watu katika sekta ya afya na kuchochea mageuzi ya uchumi wa Taifa.



Utekelezaji wa ujenzi wa Kampasi ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Mloganzila, unatekelezwa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (Higher Education for Economic Transformation – HEET).