
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ni mradi mkubwa wa kimkakati unaolenga kubadilisha mfumo mzima wa elimu ya juu nchini na kuufanya kuwa injini ya uchumi wa kisasa.

Prof. Mkenda ametoa kauli hiyo Disemba 15, 2025 mkoani Kagera, wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Kampasi ya Kagera ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Amesema kupitia mradi wa HEET, Serikali inajenga kampasi 16 za Vyuo Vikuu vya umma katika mikoa 15 ambayo awali haikuwa na Vyuo Vikuu, hatua inayolenga kusogeza huduma za elimu ya juu karibu na wananchi.

Ameitaja mikoa mingine inayonufaika na mradi huo kuwa ni Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Katavi, Kigoma, Singida, Manyara, Njombe, Ruvuma, Rukwa, Lindi pamoja na Zanzibar.

Waziri Mkenda amebainisha kuwa ujenzi wa Kampasi ya Kagera utaongeza fursa za udahili kwa wanafunzi, kuchochea ukuaji wa uchumi wa eneo husika na kuimarisha matumizi ya teknolojia pamoja na tafiti katika Kanda ya Ziwa. Aidha, kampasi hiyo inatarajiwa kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya elimu na sekta za uzalishaji.


