Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amesema Serikali itaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika elimu ya ufundi ili kuongeza ujuzi, ubunifu na ushindani wa vijana katika soko la ajira la ndani na kimataifa.



Akizungumza Desemba 15, 2025 jijini Mwanza katika Mahafali ya 19, Duru ya Pili ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Kampasi ya Mwanza, Mhe. Ameir amesema Serikali, kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kupitia mradi wa EASTRIP, imewekeza Dola za Marekani milioni 16.25 (sawa na TZS bilioni 37) kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya kufundishia teknolojia ya ngozi katika Kampasi ya DIT Mwanza.



Kiongozi huyo amesema kuwa kupitia mradi wa mwingine wa TELMS II, kiasi cha Euro milioni 5.33 (TZS bilioni 15.27) kimetengwa kwa ajili ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia ili kuongeza ubora wa mafunzo.



Katika kupanua wigo wa upatikanaji wa elimu ya ufundi, Mhe. Ameir amesema Serikali imeongeza udahili wa wanafunzi kutoka 161,750 mwaka 2023/2024 hadi 199,118 mwaka 2024/2025, sambamba na ongezeko la vyuo kutoka 441 hadi 512.



Ameongeza kuwa Serikali imewajengea uwezo wakufunzi 912 katika ufundishaji wa mitaala ya umahiri, huku wakufunzi 45 wakipatiwa mafunzo ya teknolojia mpya za mnyororo wa thamani wa sekta ya ngozi ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira.



Amesema kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali imepanga kutoa ithibati kwa vyuo 70 zaidi ili kufikisha jumla ya vyuo 582 vya elimu ya ufundi na ufundi stadi, pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu 1,000 na kuhuisha tathmini ya mitaala ya umahiri.



Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, amesema Serikali imejidhatiti kuendelea kuwekeza kwa vijana kupitia elimu, hususan Elimu ya Ufundi na Teknolojia, ili kujenga rasilimaliwatu yenye ujuzi na uwezo wa kushindana katika soko la ajira



Prof. Mushi alisema dhamira hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuhakikisha vijana wanaandaliwa ipasavyo kutekeleza ajenda za taifa ambazo ni maendeleo ya viwanda, uchumi wa kidijitali, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu