Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,Dkt. Hussein Omari, amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika kukuza vipaji vya vijana kupitia elimu, akisema juhudi hizo zinawajenga kuwa kizazi kinachofikiri kwa kina na chenye mchango kwa taifa.



Dkt.Omari ameyasema hayo Oktoba 26, 2025 jijini Dodoma, wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo kwa washindi wa mashindano ya uandishi wa insha za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na SADC, ambapo wanafunzi kutoka shule mbalimbali walipewa zawadi kwa ubunifu na uwezo wao wa kuandika.



Amesema mashindano hayo yanasaidia kujenga uzalendo miongoni mwa vijana na kuwahamasisha kutumia teknolojia kwa njia chanya inayokuza fikra tunduizi.



Aidha, amewapongeza walimu na wazazi kwa kuwaandaa vizuri wanafunzi na amewahimiza wanafunzi nchini kote kuendelea kushiriki mashindano kama haya ili kukuza vipaji vyao zaidi.



“Tunawafundisha vijana kufikiri zaidi, jambo ambalo litakuwa tunda jena kwa kizazi kijacho. Hii ni njia mojawapo ya kukuza uzalendo na kuwaandaa kuwa raia wenye mchango chanya kwa taifa,” amesema Dkt.Omari