Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa elimu inaendelea kutekeleza mikakati kabambe ili kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023 kwa mafanikio.



Akifunga Mkutano wa Mwaka wa Tathmini ya Pamoja ya Sekta ya Elimu 2024/25 jijini Dodoma Oktoba 24, 2025, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema Serikali inajivunia mafanikio mengi katika sekta ya elimu na imejipanga kuongeza fursa za kuboresha elimu, ikiwemo kuongeza idadi ya walimu wa sayansi, biashara na masomo ya ufundi.



"Tutaimarisha na kuongeza matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji na kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali kwa ajili ya elimu" amesema Katibu Mkuu.



Amewashukuru wadau wote kwa ushirikiano mzuri na amewapongeza walimu wote wa ngazi mbalimbali kwa kazi nzuri wanayofanya.


"Hakuna elimu bila mwalimu, kwani ndio msingi wa kujenga nguvu kazi ya Tanzania yenye maarifa na ujuzi na kuwa tayari kushinda katika solo la ajira kitaifa na Kimaraifa" Ameeleza Prof. Nombo