Mwakilishi wa Ubalozi wa Uingereza, Godfrida Magubo, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu katika ngazi zote za elimu ambayo imechochea ufundishaji na ujifunzaji.

Magubo amesema hayo Oktoba 22, 2025 jijini Dodoma katika Mkutano wa Mwaka wa Tathimini ya Sekta ya Elimu, ambapo amesisitiza matumizi ya teknolojia na takwimu sahihi ili kuwezesha kufuatilia maendeleo ya elimu.



Ameahidi kuwa Serikali ya Uingereza itaendelea kushirikiana na Serikali katika kukuza elimu jumuishi na endelevu.



Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Elimu Tanzania (TENMET), Simon Nanyaro, amesema Mkutano huo ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa sera, mipango na miradi ya elimu.



Naye, Mwakilishi wa Jumuiya za Kidini kutoka Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Dkt. Joyce Mboya, amesema kama wadau muhimu wapo tayari kushirikiana na Serikali kuhakikisha kuwa kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu bora itakayomwandaa kwa maisha na kazi.