
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, amesema kuwa Serikali inaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali katika kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, ili kuhakikisha elimu inayotolewa inakidhi mahitaji ya sasa na baadae ya kijamii na kiuchumi.

Prof. Mushi ameeleza hayo Oktoba 22, 2025 jijini Dodoma akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya kufungua Mkutano wa Mwaka wa Tathmini ya pamoja ya Sekta ya Elimu, 2024/25 unaolenga kutathmini mafanikio yaliyopatikana, kubaini changamoto na kupanga mikakati kabambe ya utekelezaji wa mageuzi ya elimu.

Ameongeza kuwa, katika kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia, Serikali kupitia Wizara imejielekeza katika kukuza elimu inayolenga kutoa maarifa na ujuzi unaohitajika katika karne ya 21, ili kuliwezesha taifa kupata wahitimu mahiri wanaoweza kushindana kikamilifu katika soko la ajira la ndani na kimataifa.

“Kuna ongezeko la rasilimali, ongezeko la miundombinu, Serikali haiwezi pekee yake kuwezesha mahitaji haya yote, ndiyo maana inakutana na wadau mbalimbali kujadili na kupanga juu ya maeneo na namna nzuri ya kuwekeza katika elimu ili kufikia lengo la kuandaa rasimali watu mahiri ambao ni mtaji mkubwa katika kufikia Dira 2050,” amesema Prof. Mushi.


