Serikali inaendelea kuwekeza katika elimu ya ufundi na ufundi stadi ili kuandaa vijana wenye ujuzi, umahiri na ubunifu unaokidhi mahitaji ya soko la ajira. Akizungumza Oktoba 17, 2025 jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema mfumo wa elimu unalenga kuandaa wahitimu wenye ushindani wa kimataifa na uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa ndani na nje ya nchi.



Prof. Nombo amesema Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, imeweka mkazo katika mafunzo ya ujuzi.

VETA imeboresha mitaala, miundombinu na mbinu za ufundishaji. Kwa sasa kuna zaidi ya vyuo 900 vinavyodahili wanafunzi 300,000 kwa mwaka, huku vyuo vingine 64 vikiendelea kujengwa katika ngazi ya wilaya.



Aidha, serikali imeimarisha ushirikiano na sekta binafsi na mashirika ya kimataifa kama Benki ya Dunia, Umoja wa Ulaya, GIZ na KOICA. Ushirikiano huu umewezesha mafunzo ya vitendo, vifaa vya kisasa, mitaji midogo kwa wahitimu na vyeti vya utambuzi wa kitaalamu.



Prof. Nombo ametoa wito kwa wadau wa viwanda kushirikiana na taasisi za elimu kuendeleza bunifu za vijana hadi kufikia uzalishaji na biashara.