Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuendelea kupanua wigo wa upatikanaji wa Elimu ya Watu Wazima nchini.



Mhe. Majaliwa ametoa wito huo Agosti 25, 2025 Jijini Dar es Salaam katika Kilele cha Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 50 ya Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi bila kujali hali zao za kiuchumi, umri au mahali walipo.



Katika hotuba yake, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa Elimu ya Watu Wazima ni nyenzo muhimu ya kuwajengea Watanzania uwezo wa kujikomboa kiuchumi na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.



Ameeleza kuwa fursa za elimu zinapaswa kuwa jumuishi na zenye kuzingatia mahitaji halisi ya jamii, ili kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika safari ya kujifunza na kujijenga.



Aidha, Mhe. Majaliwa ameitaka Wizara kushirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali wa elimu ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika vituo vya elimu bila ukomo, ikiwemo kuwekeza katika miundombinu bora pamoja na vifaa vya kisasa vinavyowezesha utoaji wa elimu kwa ufanisi na kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya walengwa.



Kauli ya Waziri Mkuu ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya kuendeleza elimu jumuishi na endelevu, inayolenga kuwafikia Watanzania wote bila ubaguzi. Ni mwito wa kuchukua hatua madhubuti katika kuimarisha Elimu ya Watu Wazima kama sehemu ya msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.