
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Akutana na Viongozi wa TET na Kamati ya Tuzo ya Uandishi Bunifu ya Mwalimu Nyerere
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amekutana na kufanya mazungumzo na Baraza la Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) linaloongozwa na Mwenyekiti wake, Prof. Maulid Mwatawala, kujadili uendeshaji wa masuala mbalimbali ya taasisi hiyo.
Katika kikao hicho, Prof. Mkenda amesisitiza umuhimu wa kuendeleza ubora wa utendaji na kuhakikisha taasisi inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kwa kuzingatia mahitaji ya sekta ya elimu nchini.
Aidha, Waziri Mkenda amekutana na Kamati ya Kitaifa ya Uandaaji wa Tuzo ya Uandishi Bunifu ya Mwalimu Nyerere, inayoongozwa na Prof. Penina Mlama, ambapo walijadili masuala mbalimbali yanayohusu maandalizi na utekelezaji wa tuzo hiyo muhimu kwa kuenzi mchango wa Mwalimu Nyerere katika taaluma ya uandishi na elimu.
Katika vikao hivyo viwili vilivyofanyika kwa nyakati tofauti leo, Waziri Mkenda amepongeza Baraza la TET na Kamati ya Tuzo kwa utendaji mzuri wa kazi unaoendelea kufanyika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la TET, Prof. Mwatawala, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuiwezesha taasisi hiyo kutekeleza majukumu yake ya kikazi kwa mafanikio.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo, Prof. Penina Mlama, amemhakikishia Waziri kuwa kamati yake itaendelea kufanya kazi kwa weledi, ubunifu, na kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.