Katika kuimarisha usimamizi wa elimu ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu nchini, Naibu Katibu Mkuu Prof. Daniel Mushi Agosti 29,2025 amefanya ziara ya kikazi katika Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) jijini Dar es Salaam.



Ziara hiyo ililenga kuweka Kwa pamoja mikakati ya kuendeleza elimu ya juu ili iwe ya ushindani wa kikanda na kimataifa.



Katika mazungumzo na uongozi wa TCU, Prof. Mushi alisisitiza umuhimu wa kuwa na mifumo madhubuti ya kuratibu elimu ya juu ili kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi, maadili, na uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira la kisasa.



Alibainisha kuwa ongezeko la wanafunzi wa vyuo vikuu linahitaji sera na miundombinu inayoweza kuhimili kasi ya mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya karne ya 21.



Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) alimshukuru Naibu Katibu Mkuu, Profesa Daniel Mushi, kwa maelekezo aliyotoa ambayo yameonyesha maeneo ambayo kifanyiwa kazi yataongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Tume hiyo