
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaendelea na ujenzi wa miundombinu mipya katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST). Uwepo wa majengo haya Chuo kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 30,000 kutoka 13,000 ilivyo sasa.
Ujenzi wa miundombinu hiyo unafadhiliwa na Serikali kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ambao ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia na unahusisha ujenzi wa Jengo la taaluma lenye madarasa, ofisi, maabara mbili za Kompyuta, na maabara za uhandisi.
Miundombinu mengine ni karakana nne zenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi zaidi ya 600 kwa wakati mmoja, pamoja na kituo cha ubunifu na uhaulishaji wa teknolojia ( _Center for Innovation and Technology Transfer_ ), majengo ambayo yataboresha mazingira ya mafunzo.
Miundombinu hiyo yote inajengwa katika kampasi kuu ya chuo hicho, iliyoko Mbeya, kwa gharama ya zaidi ya bilioni 16, hatua hii inalenga kuimarisha ubora, kuongeza fursa za elimu ya juu na mchango wa elimu ya juu katika maendeleo ya taifa.