Na WyEST Dar es Salaam

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanzisha Mfuko wa Mikopo nafuu ya Ubiasharishaji Bunifu Tanzania utakaojulikana kwa Jina la *Samia Fund*

Hayo yameelezwa Jijini Dar es Salaa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati wa ufunguzi wa Kongamano na Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ambapo amesema kuwa Mfuko huo uliopata fedha kutoka kwenye Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) utawasaidia vijana wabunifu kupata mitaji ya kuingiza sokoni bunifu zao.



Prof. Mkenda ameongeza kuwa imekuwa kawaida ya wabunifu kuonyesha bunifu katika maonesho mbalimbali lakini hazifiki katika soko ili ziweze kutumika na kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii kutokana na kukosa mitaji.



Waziri huyo amesema ili kuhakikisha mfuko huo unakuwa endelevu serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaendelea kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali ikiwemo mabenki ambapo mpaka sasa Benki ya CRDB imeonyesha mwelekeo mzuri wa kuingia mkataba na Serikali ili kusaidia wabunifu.



Aidha, Prof. Mkenda amesema kuwa ili kuwasaidia watafiti watakaojikita katika kufanya tafiti za mabadiliko ya Tabianchi Serikali ya watu wa Norway imetoa ufadhili wa shilingi Bilioni 6.3 kuwasaidia watafiti 19.